Kauli kali na tata aliyotoa mshairi mheshimiwa Taban Lo Liyong miaka ya sitini kuwa Afrika Mashariki ni ‘jangwa kifasihi’ imetawala mijadala nyingi kuhusu uwezo wa Mwafrika kubuni sanaa. Mjadala ufuatao wa wapenzi wa fasihi ya Kiswahili ulianzishwa na malalamiko ya Papa Were kuwa ukiritimba umekithiri fasihi ya Kiswahili. Ni mjadala unaofaa kuendelezwa na zaidi ya maoni ya hawa wasomaji wachache na wachanga.
Papa Were: Riwaya na hadithi fupi si chochote zaidi ya kauli zilizochujuka kwa kutumiwa zaidi hivyo kuchosha. Pengine huku ‘kukwama’ ndiyo nembo ya fasihi yetu. Yamkini hili humfanya Taban kusema vile. Ama tatizo ni kusoma kwetu kwa miwani ya mitazamo ya magharibi? Tatizo ni usomi au uandishi?
Nyamweya Bw’Omari: Wasomaji wamechangia kifo cha hii fasihi ‘yetu’. Kwingineko, mwalimu mmoja (wa Kiswahili) amekiri kuwa hasomi tena riwaya za Kiswahili kwa sababu ni ghushi. Fasihi isiwe mbovu au mbaya kwa sababu ya waandishi wawili watatu wabinafsi.
Papa Were: Nililia baada ya kusoma Nasikia Sauti ya Mama cha Ken Walibora hivi karibuni. Kazi hiyo ilizoa Tuzo la Jomo Kenyatta la 2015 (imepachikwa katika jalada). Je, kitabu hiki kilishinda kwa kuwa yu bora zaidi au jina lake Walibora liliburuta wanajopo waliotathmini vitabu vilivyowasilishwa kutuzwa? Huenda ni wanamauzo walitaka kutumia jina la Walibora kupata donge nono? Iwapo Profesa ni mzuri kweli, kwa mujibu wa tuzo hili, hili laiweka wapi fasihi ya Kiswahili? Fasihi hii inaelekea wapi?
Victor Bw’Omimi: PapaWere, naipata mantiki yako vyema. Tatizo ni kuwa baadhi ya tuzo zimejaa ufisadi. Tunaangalia jina la mwandishi badala ya kazi. Kiukweli zipo kazi nzito zinazofaa tuzo ila haziwezi kupata mwanga wa asubuhi kwa sababu waandishi wake ‘hawajulikani’.
Apa Mwambeo: Naona Taban Lo Liyong ni mwenye mapendo sana kutuita jangwa kifasihi. Naamini tu zaidi ya jangwa. Hali yetu ni ajali ya kifasihi kwa kuwa kazi nyingi za Kiswahili zinasikitisha.
Victor Bw’Omimi: Kinyume na ilivyo katika fasihi nyingine ni kuwa fasihi ya Kiswahili imefanywa kuegemea kusoma kazi ya mtu mmoja tu. Sasa malezi ndiyo shida. Kwa mfano, Kezilahabi alituachia nani arithi wino na ueledi wa kazi aliokuwa nao?
Nyamweya Bw’Omari: Victor Bw’Omimi, unakumbuka Tata za Asumini. Hiyo ni riwaya na nusu. Ukimsoma S. A. Mohamed katika Babu Alipofufuka au Nyuso za Mwanamke, hutafurahia kazi ikiwa hutatumia jicho la kinadharia. Bayana tujadiliane, ni kigezo kipi tutatumia kusema kazi (ya fasihi) ni chapwa? Karne ya ishirini na moja ina kazi nyingi tu zenye mashiko.
Apa Mwambeo: Angalia Chozi la Heri cha Assumpta K. Matei, kwa mfano. Mbona ajali kama hii iruhusiwe kuwa kitabu seti kwa umri tunaokusudiwa kuuchochea na upendo kwa fasihi? Mtu ataipendaje fasihi akishakutana na kazi kama hii? Idadi kubwa ya wahusika na ule ubadhirifu wa sadfa ndani ya kazi hii, nisitaje mkolezo wa msamiati wa Kiswahili, ni dhiki.
Victor Bw’Omimi: Wanakiita Chozi la Heri. Ni chozi kweli. Unajua kazi kama hii ndiyo inafanya watu wapige fasihi ya Kiswahili. Hata hivyo, kama lugha nyingine, ndipo fasihi ya Kiswahili imepiga hatua. Ingawa haijafika kiwango cha ile ya Kiingereza, matumaini yapo.
Papa Were: Kubwabwaja huku kulikuwa na dhamira ya kuyatumia maamuzi ya majopo ya fasihi na sanaa kama ratili ya kupima uzito wa sanaa yetu. Kilichotatiza ni kuwa Naskia Sauti ya Mama kilipata tuzo ya JKF. Kwa vigezo vipi? Kweli zipo kazi nzito za baada ya mwaka wa 2000. Je, Naskia Sauti ya Mama ni mojawapo (kwa kuzingatia vigezo anuwai, na vya binafsi, vya ukuu wa jungu letu)? Je, JKF wakisimama mbele ya wasomaji na wasomi wa fasihi ya Kiswahili, kuna imani kuwa wataweza kuitetea tuzo hii?
Apa Mwambeo: Hatutazamii kusisimuliwa au kuchachawizwa na nyingi ya kazi za Kiswahili za kileo. Kubwa mle ni maneno magumu, sadfa, kukidhi nadharia, kushindilia mbinu za lugha na upuzi kama huo. Hiki ni kitanzi kwa ubunifu.
Victor Bw’Omimi: Hizo kazi za miaka za 2000 zina mashiko, hasa za S. A. Mohammed na Kezilahabi. Tatizo lingine ni kwamba waandishi chipukizi hawajaandika kazi komavu kama hizo. Tatizo la wengine ni kuweka fasihi ya Kiswahili kiwango cha fasihi za Kiingereza. Ukisoma kazi ya fasihi ya Kiswahili na mtizamo wa fasihi ya Kiingereza basi hautapata ulichodhamiria.
Apa Mwambeo: Tulaumu umri? Kizuri hutambulika kingali utotoni. Naona hatuivi hata kwa karne kadha. Tumevumbikwa tu, twavunda.
Nyamweya Bw’Omari: Apa, swali la umri ni swali nzuri. Iweje mtoto wa umri wa miaka kumi na miwili ale chakula cha mtu kama mimi au wewe mwenye miaka 42? Itawezekana uwe na maarifa zaidi ya aliyonayo Mzee Kibor kuhusu ndoa? Ikumbukwe kuwa fasihi ya kwingineko imehakikiwa kwa muda mrefu tena na watu wengi. Hatujajitahidi kubuni nadharia au vifaa vya kusoma fasihi ya Kiswahili. Pengine tunatumia pembejeo zisizofaa. Kazi kwa Mwarabu, malipo kwa Mhindi.
Victor Bw’Omimi: Wajua wanaozisoma bila nadharia wanaziona ghushi ila huo ughushi ukiwauliza wauseme wataegemea Kiingereza. Wapo waandishi wengi wa fasihi. Tatizo ni kuwa hawajapata umaarufu na uwanja wa kuweka kazi zao zisomwe zaidi.
Nyamweya Bw’Omari: Unajua sababu gani Siku Njema ilipendwa na wengi? Kando na kuwa riwaya seti, haikuwa imejikita kwa ‘nadharia’. Ilikuwa na ubikra. Wangapi wanapenda Walenisi cha Katama? Mbona ni wachache na ilikuwa seti pia? Sababu kuu ya kutopata ufunguo kuiingia ni kutokuwepo utafiti na uhakiki wa kina. Ufunguo haupo.
Papa Were: Kwa mtazamo wangu, Siku Njema kilipendwa kwa sababu kililenga udhaifu wa hisia za binadamu katika kuyasawiri matatizo ya mfumojamii wa wakati huo. Haya, pamoja na ufasaha wa lugha ya simulizi, huenda yalimduwaza mhakiki wa nadharia na msomaji wa kawaida.
Apa Mwambeo: Kusuka kazi zenye kina kama za akina Shaaban bin Robert, Leo Tolstoy, Arundhati Roy na waandishi wengine huhitaji nidhamu na subira ya hali ya juu. Pupa yetu kupakua vitu vibichi na ule ukosefu nidhamu unaodhihirishwa ni ufisadi na uporaji wa kipofu unaakisi hata katika kazi bunifu. Watu wako mbioni kuwahi soko. Kisha, anavyosema Bw’Omimi, watajiingiza kwa mamluki wa mitaala ili kuhakikisha kazi zao zinamulikwa na wahadhiri wa vyuo. Isitoshe, ukweli kwamba waandishi wengi ni wahadhiri na waalimu haunikai vizuri. Si rahisi kupata uhakiki wa kina kuhusu kazi fulani wala kupuuza nyingine kwa udhaifu wao. Hii ni kwa sababu ya uhusiano wa walio katika ulingo wa fasihi ya Kiswahili.
Papa Were: Ken Walibora amewarudisha wasomi na wasomaji katika msitu wa kiza kisichotarajia macheo. Hakuna tofauti yake na Myahudi aliyemsaliti masihi kwa ndururu tatu! Kwa kuikubali tuzo ya aina hii, mwandishi alijibandika alama ya msaliti. Wengi wa wandani wangu wasomao fasihi ya Kiswahili wanajua Walibora ameandika Siku Njema tu, na kwamba Kilio cha Haki ni ususi wa Mazrui. Walimu wengi wa fasihi pia hufika hapa. Kwani, haitoshi kuchukua miongozo kwa kuwa matini zasinya? Pengine Katama Mkangi ndiye nguli aliyebirua mawazo kupitia Walenisi na Ningekuwa na Uwezo kisha akatoweka. Nimechoka kupongeza Amezidi kwa kuwa hakuna wenzake miongoni mwa riwaya.
Victor Bw’Omimi: Tunahitaji mchango zaidi. Lakini cha mno mashirika ya uchapishaji yatupe kazi mpya ili waandishi wakue. Hapo ndipo penye msitu hasa.
Papa Were: Sisi kama wahakiki wavivu twaweza kulaumu sekta ya uchapishaji kwa kutoinua waandishi limbukeni ama kwa kushirikiana na ‘wahafidhina’ kwa kisingizio cha waandishi waliobobea ili wapate kitu kidogo. Hata hivyo, vyuo havijafanya chochote miongoni mwa wakongwe na wachanga wao. Uhakiki utesao wanafunzi na walimu hadi leo ni kukamua maudhui na mbinu za lugha. Wengi walipita mtihani kwa kuteuka nadharia pasi na kujua kuzitumia. Ikiwa wahakiki ni hawa, wahakikiwa watafikapi? Ama huku ndiko kuwaandaa wahakiki kwa kazi zinazosinya huku ‘nje’?
Mjadala unaendelea. Maoni yako yakaribishwa. Wasiliana na editor@nairobibookshelf.com.
Leave a Reply